TAMKO LA ASASI ZA KIRAIA ARUSHA, KUHUSU MCHAKATO WA KUANDIKA KATIBA MPYA YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

Mahali: Ukumbi wa ANGONET Tarehe: 8/10/2013

UTANGULIZI

Arusha NGO Network (ANGONET) ni Mtandao wa kitaasisi wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali (AZISE) na yale ya Kijamii (AZAKI) Mkoani Arusha. Katika kufikia malengo yake, ANGONET inalenga kuimarisha uwezo wa AZAKI/AZISE, wadau wa maendeleo na jamii kwa ujumla katika maeneo ya usimamizi wa maliasili na uendelezaji wa mazingira; utafiti wa kisera, uchambuzi na uchechemuzi; demokrasia, haki za binadamu na utawala bora; elimu ya uraia; teknolojia ya habari na mawasiliano hasa maeneo ya vijijini; afya kwa jamii na masuala/maeneo mengine mahususi ya kitaasisi yanayojitokeza kulingana na mabadiliko ya nyakati.

Sisi ANGONET tunapenda kutoa taarifa kwa umma kupitia waandishi wa habari na vyombo vya habari kwa ujumla kuhusu masuala mbalimbali na mwenendo wa mchakato wa kuandika Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tamko letu lina mambo makuu mawili;

Mosi, ni kuhusu masuala muhimu yaliyojadiliwa na AZAKI kwa ajili ya kuboresha Rasimu ya kwanza ya Katiba kupitia Mabaraza ya Katiba yaliyoratibiwa na ANGONET.

Pili, ni kuhusu Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Namba 8, Sura ya 83 toleo lililorekebishwa la mwaka 2012 ikisomwa sambamba na Muswada wa marekebisho ya Sheria hiyo ulipitishwa Bungeni mwanzoni mwa mwezi Septemba 2013, sehemu ya tano kifungu cha 22 kinachohusu Bunge maalum la Katiba.

MASUALA MUHIMU KUBORESHA RASIMU YA KWANZA YA KATIBA

Kama ilivyo kwenye utangulizi tunatoa taarifa kwa umma na kusisitiza Tume ya Mabadiliko ya Katiba isome maoni yetu kwa umakini ili kuwezesha kutayarisha Rasimu ya pili ya Katiba. Baadhi ya mambo ya msingi ambayo yaliyopendekezwa na kusisitizwa na Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Asasi yaliyoratibiwa na ANGONET ni kama yafuatayo;

Muundo wa Muungano: Sura ya sita, Ibara ya 57 ya Rasimu ya kwanza ya Katiba inaainisha muundo wa muungano wa Serikali tatu. Uchambuzi unaonesha mfumo wa Serikali tatu katika Nchi hii ni kurudi nyuma, kuanzia 1964 mpaka 2013 ni takribani miaka 50, matarajio ni kuona tunazungumzia Taifa/Nchi moja na Serikali moja. Ilipendekezwa Muungano uunde nchi moja na washirika ambao awali zilijulikana kama nchi huru, Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya watu wa Zanzibar zitambulike kuwa dola mbili ndogo yaani dola za Tanganyika na Zanzibar na Jamhuri ya Muungano kuwa dola kuu. Hii ni kujenga maono ya umoja na utaifa.

Umiliki mali (inayohamishika na isiyohamishika): Migogoro ya ardhi, haki ya kumiliki na kutumia ardhi imekuwa ni tatizo kubwa na ajenda kuu ya kitaifa. Ardhi imekuwa inatwaliwa kwa matumizi ya umma sambamba na raia kuondolewa bila ridhaa kwa fidia isiyolingana na hali halisi na wakati mwingine bila fidia kabisa. Ilipendekezwa katika Sura ya nne, sehemu ya kwanza Ibara ya 36(2) itamke wazi kuwa “Endapo ardhi ya mtu itahitajika kwa maslahi ya umma au yoyote yale, mtu huyo atatoa ardhi hiyo kwa ridhaa yake na kwa malipo yanayolingana na thamani halisi ya mali hiyo na yatakayotolewa mapema”.

Zaidi; ardhi na rasilimali asili zingine: Rasimu ya kwanza haikuipa kipaumbele kwa ujumla wake na kwa kuzingatia muundo wa muungano unaopendekezwa, ardhi ndiyo nchi na haiwezekani kuwa na nchi bila ardhi na kwa hiyo bila ardhi hatuna Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ilipendekezwa kuongezwa sehemu au sura mpya mahususi itakayozungumzia ANGONET 

masuala ya ardhi na rasilimali zingine kwa kina ili kuhakikisha utekelezaji wa malengo ya Taifa kama yalivyowekwa katika ibara ya 7 (d) na (h) na kwamba;

Ardhi yote ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni mali ya raia wa Tanzania kwa ujumla wao kama Taifa, Kijiji, jamii au Kikundi.

Wazawa watakuwa na haki ya kumiliki na kutumia ardhi wakati wageni/wasio wazawa watakuwa na haki ya kutumia tu ardhi lakini sio kumiliki.

Mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Washirika wake iwe bayana.

Kwa Upande wa Maliasili na Mazingira

Maliasili za Taifa zitasimamiwa na kutumiwa kwa namna ambayo zitaleta tija kwa Taifa na kuwa hakutakuwa na kundi ambalo litanufaika zaidi ya jingine.

Shughuli zote za uhifadhi na mazingira zisihatarishe haki za jamii kumiliki mali, kuthaminiwa utu, kuishi, kuwa na usalama wa chakula, kuwa na makazi bora pamoja na hifadhi ya jamii na kwamba siku zote hadhi ya raia itakuwa ni zaidi ya maliasili.

Uwekezaji wowote katika mali asili uzingatie maslahi ya Taifa na raia kwanza (maendeleo ya watu kwanza).

Haki ya kupata huduma bora za afya na elimu: Suala la huduma za jamii ni kwa manufaa ya watanzania wote kwani wote ni walipa kodi. Ilipendekezwa kuongezwa ibara mahususi katika sura ya nne, sehemu ya kwanza itakayozungumzia na kubainisha wazi haki ya kila raia wa Tanzania kupata huduma bora za elimu na afya katika misingi isiyo ya ubaguzi.

MAREKEBISHO YA SHERIA YA MABADILIKO YA KATIBA

Sheria ya mabadiliko ya Katiba sura ya 83 toleo la mwaka 2012 ilipitishwa na Bunge la Jamhuri ya Mungano wa Tazanania kwa lengo la kuwezesha uandikaji wa Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (JMT). Katika kikao cha Bunge la JMT lililokaa mapema mwezi Septemba 2013, pamoja na masuala mengine Bunge lilifanya marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sehemu ya Tano inayohusu Bunge Maalum.

Kwa mujibu wa kifungu cha 22(1) cha Sheria ya mabadiliko ya Katiba, Bunge Maalum litakuwa na jumla ya wajumbe 604, yaani Wabunge 357, Wawakilishi 81 na wajumbe 166 wanaowakilisha makundi mbali mbali ya kijamii.

Uchambuzi unaonesha kifungu hiki cha Sheria kinatoa fursa finyu ya uwakilishi kwa wadau walio wengi na kumpa Rais mamlaka ya mwisho ya kuteua Wajumbe 166 wanaowakilisha makundi ya kijamii na Taasisi mbalimbali. Kutokana na hali hiyo, ni wazi kuwa nia na dhamira safi ya kuwezesha upatikanaji wa Katiba imepotea jambo ambalo kimsingi halikubaliki.

Sisi Asasi za Kiraia, Arusha tunaona sio vyema na sio busara Rais kuteuwa wawakilishi 166 wa Asasi Zisizo za Kiserikali na makundi mengine nane kama yalivyoainishwa katika kifungu cha 22(c) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Tunaamini Asasi za Kiraia na makundi mengine yanaweza kufanya hivyo na kumpata wanaemwamini kuwawakilisha. Kama Asasi hizi zilivyoshiriki katika uendeshaji wa Mabaraza ya Katiba ya Asasi vivyo hivyo zishikiki katika mchakato wa kuwapata wajumbe wa Bunge maalum. Asasi za Kiraia na makundi mbalimbali ya kijamii katika Mkoa wa Arusha kwa ujumla, tungetaka kuona mabadiliko chanya ya Muswada wa Marekebisho ya Sheria yatakayoboresha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.

Kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Wabunge wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar ni wajumbe wa Bunge maalum la Katiba ambao ni zaidi ya theluthi mbili na hii matokeo yake ni kuwa kwa vyovyote vile upigaji kura utakuwa wa msukumo na utaegemea hisia na itikadi za vyama kuliko Katiba ya Nchi. Ieleweke kuwa, wabunge wanashiriki katika shughuli za kibunge kwa muda wa miaka mitano na hawakukusudiwa kwa lengo la kuwa wabunge wa Bunge la Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Sisi tunapendekeza kuwa theluthi moja itokane na wabunge/wawakilishi, nyingine itokane na Asasi na theluthi ya mwisho iwe itokane na umma kwa ujumla wake.

HITIMISHO

Kwa kuwa Muswada wa marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba hautakuwa sheria mpaka Rais atakaposaini. Na kwa kuzingatia Muswada huo una ukiukwaji wa wazi wa haki ya ushiriki wa wananchi ambao ndio msingi unoipa uhalali mamlaka ya Serikali, sisi Mtandao wa Mashirika Yasiyo ya

kiserikali Mkoa wa Arusha (ANGONET), Mitandao ya Wilaya, wanachama wake na wapenda haki na maendeleo tunawataka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Bunge kuangalia Muswada huo kwa namna ambayo itaondoa mapungufu ya wazi ambayo hayatawezesha upatanaji wa katiba bora Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Imetolewa na:

Arusha NGO Network (ANGONET)

Rudolf Filemon

Idara ya Habari na Mawasiliano